Header Ads

KAMATI ya Kuchunguza utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa imekabidhi rasmi ripoti


KAMATI ya Kuchunguza utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa imekabidhi rasmi ripoti yake serikalini huku ikibaini sababu kuu nane za utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki jijini Mwanza na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza utoroshaji wa madini nje ya nchi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, John Bina alipokuwa akiwasilisha matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo iliyoundwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wanunuzi na wachimbaji wadogo wa madini.
Akiwa katika ziara ya kikazi jijini Mwanza, Naibu Waziri Nyongo aliunda kamati hiyo kwa lengo la kuangalia namna bora ya kudhibiti utoroshwaji wa madini kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria na namna bora ya uanzishwaji wa soko la kimataifa la madini jijini Mwanza.
Bina ambaye pia ni Rais wa Wachimbaji Wadogo nchini, alisema baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na wajumbe 17 wa kamati hiyo, ilibaini kutokuwepo kwa mfumo madhubuti wa udhibiti wa aina mbalimbali za madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo kuanzia kwenye maeneo ya uzalishaji hadi kwenye soko.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni kutotambulika kwa wachimbaji wadogo ambao sio rasmi kwenye mfumo wa kisheria na kikanuni, kuwepo kwa wingi wa kodi na utozaji wa aina moja zaidi ya mara moja, utozaji wa kodi na tozo zingine zaidi ya viwango vilivyopo kisheria.
Alitoa mfano kodi ya huduma na VAT kwenye mauzo ya nje.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni wadau na baadhi ya maofisa wa serikali kukosa uzalendo kwenye shughuli za madini, mitaji midogo kwa wachimbaji, wachenjuaji na wanunuzi wa madini, benki nyingi kutotoa mikopo kwa makundi hayo na ukosefu wa elimu ya kulipa kodi na utunzaji mbovu wa kumbukumbu.
Alizitaja changamoto zinasosababisha utoroshaji wa madini kwa wachimbaji ni kuwepo kwa uhaba wa maeneo ya kuchimba ambayo mengi yamehodhiwa na kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi zenye leseni kubwa, hali inayosababisha wachimbaji wadogo kuchimba kwenye maeneo yasiyo rasmi na kuingia migogoro na wenye leseni kubwa za utafiti.
“Wachimbaji wadogo huamua kuingia makubaliano yasiyo rafiki kwao na viongozi wa vijiji na wamiliki wa mashamba kwa kuwa wengi hawana leseni za uchimbaji,” alisema Bina.
Kwa upande wa uchenjuaji wa madini, alisema wachenjuaji wanakabiliwa na utitiri wa kodi, tozo na ada kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Msanjila licha ya kuipongeza kamati kwa kazi kubwa iliyofanya, alisema serikali itaweka mazingira mazuri ya shughuli za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wote nchini.

No comments